Umewahi kufanya majaribio ya kupima intaneti nyumbani kwako na kugundua kuwa kompyuta yako inapata intaneti ya kasi zaidi kuliko simu yako ya mkononi? Hali hii inawachanganya watumiaji wengi wanaotarajia vifaa vyote kupata kiwango sawa cha intaneti kutoka kwenye kipanga njia (router) kile kile. Ingawa simu za mkononi za sasa zina teknolojia ya hali ya juu, bado zinakabiliwa na vikwazo vya kiufundi vinavyosababisha kasi ya Wi-Fi kwenye simu kuwa ndogo ikilinganishwa na kompyuta. Katika makala hii, tutachunguza sababu kuu za tofauti hii ya utendaji kazi.
Sababu kubwa inayofanya kasi ya Wi-Fi kwenye simu kupungua ni ukubwa wa eneo la ndani la kifaa. Kompyuta mpakato (laptop) au kompyuta ya mezani ina nafasi kubwa inayoruhusu kuwekwa kwa antena ndefu na nyingi zaidi. Kompyuta nyingi hutumia mfumo wa antena mbili au zaidi (MIMO), ambazo zinaweza kupokea na kutuma data kwa wakati mmoja kupitia njia tofauti.
Kwa upande mwingine, simu za mkononi zina nafasi ndogo sana ndani yake. Antena zake ni fupi na mara nyingi zimewekwa karibu sana na sehemu ambazo mikono yako inashika, jambo linaloweza kuzuia mawimbi ya intaneti kwa urahisi.
Simu hutegemea betri ndogo inayotakiwa kudumu siku nzima, hivyo mfumo wake wa uendeshaji umeundwa kubana matumizi ya nishati kwa kila njia. Mipangilio hii ya kuzuia betri isiishe haraka hupunguza nguvu inayotumiwa na kadi ya Wi-Fi iliyo ndani ya simu.
Kompyuta zikiwa zimeunganishwa na umeme wa moja kwa moja au zikiwa na betri kubwa, zina uwezo wa kuendesha kadi zao za mtandao kwa nguvu ya juu bila hofu ya kuisha chaji mapema.
Kupokea na kuchakata data za intaneti kwa kasi kubwa hula nishati na kuzalisha joto. Kompyuta zina feni na mifumo bora ya upoeshaji inayoruhusu visindikaji vyake kufanya kazi kwa kiwango cha juu bila kupata joto kali. Simu hazina feni; hiyvo, zikianza kupata joto, mfumo hupunguza kasi ya Wi-Fi kwenye simu ili kulinda vifaa vya ndani visiharibike.
Ili kupata matokeo mazuri kwenye kifaa chako cha mkononi, hakikisha uko karibu na router na umefunga programu zinazojiendesha nyuma ya mfumo ambazo zinaweza kuathiri kasi ya Wi-Fi kwenye simu yako.
Je, umewahi kuona tofauti kubwa ya kasi ya intaneti kati ya simu yako na kompyuta? Tuambie uzoefu wako kwenye sehemu ya maoni hapa chini!









